Akiwa ni mmoja kati ya watoto 36 wa Sultan Said bin Sayyid mfalme aliyetawala kote Oman pamoja na Zanzibar, alitawala Zanzibar kuanzia 1828.
Sayyida Salme alizaliwa mnamo 1844 na mama mwenye asili kutoka Circassia,kusini mwa Urusi ya sasa na kumpoteza baba yake akiwa na miaka 12 tu.
Historia yake ni ya kipekee kwani anatajwa kuwa ndie mwanamke wa kwanza Afrika ya Mashariki kujiandikia historia yake mwenyewe kwa kitabu chake alichokiita "Memoirs of an Arabian Princess from Zanzibar" cha 1886.
Kwanini aliasi familia yake ya kifalme?
Ilianzia pale aliposhiriki kwenye njama za kumpindua kaka yake Sultan Majid alierithi kiti cha ufamle baada ya kifo cha baba yao na Sultan Barghash kushika hatamu ya uongozi hata hivyo utawala huo haukudumu,serikali ilipinduliwa tena na Majid kuchukuwa madaraka kwa mara nyengine.
Hapo maisha ya Sayyida Salme yalianza kuwa ya tofauti na kuanza kujitenga mbali na masuala ya kifalme. Kinyume na taratibu za kifalme Salme akiwa na miaka 22 alianzisha mahusiano na mfanyabiashara wa Kijerumani aliyejulikana kama Rudolph Heinrich Ruete hali iliozua gumzo kwenye na familia ya kifalme na jamii ya wafanyabiashara wa kigeni.
Hali ilichafuka zaidi pale ulipodhihiri ujauzito na kugeuka kuwa mada kuu kote Zanzibar na kuchafua hali ya hewa ndipo kaka yake Sultan Sultan Majid kuamuru kusafirishwa Saudia Arabia.
Aliondokaje Zanzibar?
Kabla ya siku ya safari Sayyida Salme alitoroka Zanzibar na kukimbilia Yemen ambako alijifungua hata hivyo mtoto alifariki. Baadae aliondoka na kuelekea Ujerumani ambako aliungana tena na bwana Ruete na kufunga nae ndoa na kufanikiwa kuzaa nae watoto watatu.
Huko ndipo Sayyida Salme alibadili dini na jina lake rasmi na kuitwa Emily Ruete hata hivyo ilipofika 1870 ajali ilichukua uhai wa mume wake hali iliyomuacha kizuka wa watoto watatu. Alifariki mwaka 1924 akiwa na umri wa miaka 80 na kuzikwa hukohuko Ujerumani.
Comments