TUJIFUNZE KIDOGO

*🌹KISA CHA KUVUTIA🌹*

Mfalme mmoja aliwaamrisha wanajeshi wake kuwakusanya na kuwaua mababu wote vikongwe. Lakini alikuweko kijana mmoja anampenda sana baba yake. Aliposikia amri ya mfalme, alimficha baba yake kwenye chumba cha siri. Askari wa mfalme walipokuja, hawakupata mtu.
Siku nyingi zilipita na mfalme akagundua kuwa kijana yule amemficha baba yake nyumbani kwake. Akaamua kumtahini kijana yule kabla ya kumlazimisha aoneshe alipomfica baba yake.
Alituma watu wake kwa yule kijana na kumwambia mfalme anakwita, lakini ukienda kwake uende umepanda juu ya kitu na wakati huo huo unatembea kwa miguu. Kijana akakimbilia kwa baba yake maana alijua ni muhali kutekeleza amri ya mfalme. Baba yake alitabasamu na kumwambia chukua gongo wende nalo kwa mfalme ukiwa umelipanda na huku unatembea.
Mfalme kuona vile alishangazwa sana na akili ya yule kijana, lakini hakukubali kushindwa, akamuamrisha yule kijana aje tena kesho lakini akiwa amevaa viatu na wakati huo huo anatembea miguu chini. Akaona ni mtihani huu. Akarudi kwa baba yake. Baba akacheka, akamwambia hilo ni jambo dogo tu, chukua viatu ukate sehemu yake ya chini wende kwa mfalme ukiwa umevivaa. Mfalme alipomuoa alizidi kushangaa lakini hakukubali kushindwa. Akamwambia njoo tena kesho, lakini ukija uje na adui yako na rafiki yako. Kijana akaona sasa hii balaa, nitampata wapi adui yangu na kumkinaisha twende kwa mfalme? Akarudi kwa baba yake. Baba ambaye alikuwa anazijua vyema tabia za mke wa mwanawe na hazikumridhisha hata kidogo, tena kila siku akimshauri mwanawe amwache mke yule, lakini kijana alikuwa haoni hasikii, alimwambia mwanawe, ukienda kwa mfalme kesho, nenda na mkeo na mbwa wako. Mtoto akasema, kivipi? Akamwambia, wewe fanya nilivyokuelekeza. Ukifika kwa mfalme, mchape mkeo na mbwa wako. Akahoji, inawezekana kweli nimchape mke wangu tena mbele ya mfalme, akasema, mke mchape kidogo tu, lakini mbwa mchape sana. Kijana akaona hakuna njia nyingine ya kuokoka na panga la mfalme ila kutekeleza ushauri wa baba yake. Walipofika mbele ya mfalme, akanyanyua mkono na kufanya kama anataka kumpiga kibao kikali mkewe, yule mwanamke akaruka! Aka babu weye! Huna mwingine wa kumpiga ila miye! Kama ni kufa si ufe tu! Tena seyyid yangu mfalme, nikupe siri! Huyu bwana amepinga amri yako, amemficha baba yake kwenye chumba cha siri nyumbani. Yule kijana hakusema kitu, bali alimpiga mbwa wake kama alivyotakiwa na baba yake. Mfalme akamuuliza, unataka kututhibitishia nini?  Kijana akasema, umemsikia mke wangu alivyosema, hebu sasa mwangalie mbwa wangu atakavyofanya. Akamwita mbwa wake kwa jina alilozoea kumwita, mbwa akaja mbio huku akitikisa mkia. Kijana akasema, amri yako nimeitekeleza seyyid yangu, nimekujia leo na rafiki na adui yangu. Mfalme akashangaa sana. Akamwambia najua kuwa fikra hizi zote ni za baba yako. Kesho njoo naye asubuhi nimuone. Alipoletwa mbele yake, mfalme alimteua yule mzee kuwa mshauri wake.
Naam, vyovyote itakavyokuwa, mzazi ni mzazi, na baba ni baba na mama ni mama. Hao ni hazina kubwa kwa watoto wao.
Yaa Allah tunakuomba uwape kauli Waislamu wake kwa waume, walio hai na waliokufa. Udumishe mapenzi katika ndoa na familia zetu, tuzidi kupendana.
by king perfect